
Mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2019 si mwingine bali ni Lionel Messi, ambaye amejichukulia kinyang'anyiro cha kuwa mchezaji bora zaidi kwa mara ya sita.
Mchezaji huyo wa Argentina mwenye miaka 32 amenyakua tuzo hiyo baada ya kuikosa toka mwaka 2015 na hii ni kutokana na kuweza kufunga mara 54 katika klabu ya nchini kwake kwa mwaka 2018-19 .
Virgil van Dijk alikuwa mshindi wa pili - yeye ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Liverpool katika saba bora, akiwemo Sadio Mane.
Mchezaji wa Juventus Cristiano Ronaldo, aliwahi kutunukiwa tuzo hiyo mara tano na amekuwa watatu katika kura.
Toka mwaka 2008 tuzo hiyo maarufu zaidi ya wasakata kandanda duniani imetawaliwa na washambuliaji hatari katika kizazi cha sasa Messi na Ronaldo.
Mpaka kufikia mwaka 2017, kila mmoja wao akishinda mara tano.
Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric aliingilia ufalme wa Messi na Ronaldo baada ya kunyakua tuzo hiyo mwaka jana.
Na sasa Messi amerejea kileleni kwa kumpiku Ronaldo na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kunyakua tuzo hiyo mara sita.

Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa mwaka huu kwa Messi, Ronaldo na Van Dijk kuwania tuzo moja kwa pamoja.
Mara ya kwanza walikutana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Ulaya (Uefa) mwezi Agosti ambapo Van Dijk aliibuka na ushindi.
Mara ya pili wakaminyana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Fifa ambapo Messi aliibuka mshindi.

Tano Bora ya Ballon d'Or
1. Leonel Messi (Barcelona na Argentina)
2. Virgil van Dijk (Liverpool na Uholanzi)
3. Cristiano Ronaldo (Juventus na Ureno)
4. Sadio Mane (Liverpool na Senegali)
5. Mohammed Salah (Liverpool na Misri)
Ballon d'Or ni nini?
Tuzo ya Ballon d'Or imekuwa ikitolewa nchini Ufaransa kila mwaka toka 1956, na mshindi wake wa kwanza alikuwa mchezaji kutoka Uingereza Stanley Matthews.
Awali tuzo hiyo ilikuwa ni kwa wachezaji wa Ulaya tu kabla ya kufanyika mabadiliko mwaka 1995 na kujumuisha wachezaji wa mataifa yote duniani, mradi wanasakata kandanda katika vilabu vya Ulaya.
Orodha ya majina ya wachezaji 30 bora huandaliwa na baadae kupigiwa kura na wanahabari wa michezo kutoka sehemu tofauti duniani, ambapo kila nchi hupiga kura moja.
Kutoka mwaka 2010 mpaka 2015 tuzo hiyo iliunganishwa na ile ya Fifa lakini zilitengana mwaka 2016 ambapo Fifa ilianza kundaa tuzo zao wenyewe.
Washindi wa Ballon d'Or : Ronaldo & Messi watawala kuanzia 2008 | |||
---|---|---|---|
2008 | Cristiano Ronaldo | Lionel Messi | Fernando Torres |
2009 | Lionel Messi | Cristiano Ronaldo | Xavi |
2010 | Lionel Messi | Andres Iniesta | Xavi |
2011 | Lionel Messi | Cristiano Ronaldo | Xavi |
2012 | Lionel Messi | Cristiano Ronaldo | Andres Iniesta |
2013 | Cristiano Ronaldo | Lionel Messi | Frank Ribery |
2014 | Cristiano Ronaldo | Lionel Messi | Manuel Neuer |
2015 | Lionel Messi | Cristiano Ronaldo | Neymar |
2016 | Cristiano Ronaldo | Lionel Messi | Antoine Griezmann |
2017 | Cristiano Ronaldo | Lionel Messi | Neymar |
2018 | Luka Modric | Cristiano Ronaldo | Antoine Griezmann |
2019 | Lionel Messi | Virgil van Dijk | Cristiano Ronaldo |
No comments:
Post a Comment