Na Deric Samora
Mmoja kati ya wanafunzi wawili wa Tanzania waliotekwa nyara na wapiganaji wa Hamas wakati wa uvamizi wao Israel amefariki dunia.
Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa Clemence Felix Mtenga, mwanafunzi mwenye miaka 22, ndiye aliyefariki. Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo yan je ya Tanzania, hata hivyo haijaeleza amefariki lini, wapi na mazingira ya kifo chenyewe.
Mtenga alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wawili kutoka Tanzania ambao serikali ya Israeli hapo awali ilithibitisha kuwa wametekwa na Hamas baada ya shambulio la Oktoba 7.Serikali ya Tanzania imeeleza katika taarifa hiyo kuwa inaendelea kuwasiliana na Israeli juu ya taarifa za Mtanzania mwengine Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu mashambulizi hayo.Jumla ya watu 230 walichukuliwa mateka huku wengine 1,200 wakifariki dunia katika mashambuli hayo. Kwa mujibu wa Israel, mateka hao – ambao walipelekwa katika ukanda wa Gaza – wanatoka katika nchi 25, ikiwemo raia mmoja wa Afrika Kusini ambaye hadi sasa hajatambulika. Mpaka sasa ni mateka wanne tu ndio walioachiwa huru.Marehemu Mtenga pamoja na Mollel walikuwa ni miongoni mwa vijana 260 wa Tanzania waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Israel.Wote wawili waliwasili Isreali mwezi Septemba, wiki chache kabla ya mashambulizi ya Hamas, na programu yao ya masomo ilikuwa ya urefu wa miezi 11.Baada ya taarifa za kutekwa kwake kuthibitishwa mwezi uliopita, dada wa Mtenga aliiambia BBC Swahili kuwa familia nzima ilikuwa na hofu, lakini hata hivyo walikuwa na matumaini kuwa ataokolewa.
Aidha imewahakikishia raia wake wanaoishi katika mataifa ya kigeni ikiwemo wanafunzi waliopo katika masomo nchini Israel kuwa kupitia ubalozi wake uliopo mjini Tel Aviv, nchini Israel, itaendelea kuwasiliana na mamlaka ya taifa hilo kuhakikisha kuwa Watanzania wote waliopo nchini humo wako salama.
No comments:
Post a Comment